21.5 Jinsi ya kushughulikia mwanamke anayevuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito

Ukitambua kwamba mwanamke anavuja damu na unashuku kuwa ana plasenta iliyotengeka, privia ya plasenta, uterasi iliyopasuka, au kuvuja damu kufuatia visababishi vingine, chukua hatua hizi:

 • Usimchunguze ukeni
 • Tathmini kwa haraka hali zote za mwanamke, pamoja na dalili muhimu: mrindimo, shinikizo la damu, pumzi na halijoto, baini kama ameparara, ana uchovu, kizunguzungu, na kuchanganyikiwa.
 • Ukikisia kuwa ana mshtuko, anza matibabu haraka iwezekanavyo kwa kumdungia viowevu vya Chumvi ya Kawaida au mchanganyiko wa kiowevu cha laktesi ya Ringer ndani ya mishipa. (Utajifunza jinsi ya kufanya hivi katika somo la nadharia katika Kipindi cha 22 na kuukuza ustadi wako katika mafunzo ya kiutendaji.)
 • Hata ikiwa hakuna ishara za mshtuko, utilie mshtuko maanani huku ukiendelea kutathmini hali ya mwanamke kwa kuwa inaweza kubadilika ghafla. Ikiwa mshtuko utatokea, chukua hatua zilizoelezwa hapo juu.
 • Kwa haraka, watafute watu wakusaidie, wajulishe kuhusu uzito wa hali hiyo na utekeleze mpango wa kushughulikia matatizo ambao uliandaa wewe na mwanamke kama sehemu ya utunzaji maalum katika ujauzito (Kipindi cha 15 cha Moduli hii). Kwa mfano, watafute wanakijiji wakusaidie kumsafirisha haraka hadi kituo cha juu cha afya; hakikisha kuwa watu wenye afya njema wameandamana naye ili kumtolea damu iwapo atahitaji.

Kumbuka kuwa damu inayovuja mwanzoni inaweza kuwa nyingi sana na hatari kwa maisha, hivyo mwanamke anaweza kufika katika Kituo cha Afya akibebwa na jamaa zake. Katika hali hiyo, baada ya kufanya uchunguzi wa haraka wa hali ya mgonjwa, andaa mrija wa kudungia dawa mishipani, andaa usafiri kisha umpe rufaa haraka iwezekanavyo hadi katika kituo cha afya kilicho karibu.

 • Ni hali gani salama zaidi ya kumsafirisha mwanamke? (Rejelea Mchoro 20.3 katika kipindi cha awali)

 • Mwanamke anapaswa kukilaza kichwa chake bapa — usiweke mto chini ya kichwa chake. Mwinue magoti na umwegemeze miguuni kwa kutumia mto au blanketi iliyokunjwa, ili miguu iinuke zaidi ya kichwa chake.

  Mwanamke anapaswa kupendekezewa rufaa kila mara na ni muhimu azalie katika kituo cha hali ya juu zaidi iwapo atavuja damu katika awamu za mwisho za ujauzito, hata ikiwa damu itasita kuvuja bila usaidizi wowote kabla ya leba kuanza.

  Mwisho wa jibu

Kwa kawaida, unapaswa kuandamana na mwakamke huyu ili kudhibiti viowevu alivyotiwa na uhakikishe kuwa umeshikilia kifuko cha kiowevu juu yake. Iwapo hutaweza kwenda naye, mweleze mtu atakayeandamana naye umuhimu wa kudumisha hali ya mwanamke na kifuko katika namna iliyoelezwa; pia mweleze mtu huyu jinsi ya kufunga sindano ya kutia viowevu mishipani wakati viowevu vilivyo katika kifuko vitamalizika. Kumbuka kumpa mwanamke huyu barua ya rufaa.

Katika kipindi cha mwisho cha Moduli hii, tunakufunza kwa nadharia jinsi ya kutayarisha viowevu vinavyotiliwa mishipani, na jinsi ya kuingiza katheta ya mkojo kwa mwanamke asiyeweza kukojoa kwa sababu ya matatizo ya ujauzito au leba.

21.4 Uterasi iliyopasuka

Muhtasari wa Kipindi cha 21