22.3.2 Wakati unaofaa wa kusitisha kuingiza viowevu mshipani

Ukilinganisha na mkono mwingine, chunguza uvimbe wowote karibu na eneo la mshipa lililodungwa. Uvimbe huu unaweza kuashiria kuwa kanula imetoka na viowevu vinaingia kwenye tishu laini badala ya mshipa. Ukiona uvimbe huu, legeza plasta kisha utoe kanula. Chagua eneo jipya la kudunga mshipa kisha utumie kanula nyingine safi kudungia mshipa mwingine na uiunganishe tena na kifuko cha viowevu.

Kiowevu husitishwa kuingia mshipani iwapo mwanamke hahitaji viowevu zaidi, au sehemu iliyodungiwa kanula ikiambukizwa (ngozi iliyo karibu na eneo hili itakuwa nyekundu na mgonjwa atahisi maumivu ukimgusa). Wakati mwingine, wagonjwa wanaweza kupewa viowevu vingi kwa muda mfupi. Hatua hii inaweza kushinikiza moyo kwa sababu kiasi cha damu kimeongezeka. Pia viowevu vinaweza kuingia ndani ya mapafu, na katika matukio kama hayo mgonjwa anaweza kuwa na shida ya kupumua, kukohoa na wakati mwingine anachanganyikiwa. Jambo hili haliwezi kutokea iwapo utakuwa ukimhudumia mgonjwa huyu kwa sababu utampendekezea rufaa kwa dharura punde baada ya kuanzisha matibabu ya kupitishia viowevu mishipani. Lakini ukikabiliwa na tukio hili, unapaswa kusitisha viowevu na kumhamisha mwanamke huyo hadi kituo cha afya cha kiwango cha juu kilicho karibu ili apate matibabu zaidi.

Unaweza kusitisha viowevu kwa kufunga kigurudumu cha klampu hivyo viowevu havitashuka tena. Iache kanula ikiwa imepachikwa mkononi ili itolewe katika kituo cha afya kwa kuzingatia usafi unaohitajika.

  • Ili kusitisha upitishaji wa viowevu unahitaji glavu safi au zilizosafishwa mno, pamba safi iliyokauka, kipanguzio cha antiseptiki au pamba iliyotumbukizwa ndani ya alkoholi na plasta mpya.

Mweleze mgonjwa unachonuia kufanya, vaa glavu na 'uzime' klampu. Hakikisha kuwa mtiririko wa viowevu ndani ya mrija umesitishwa. Huku ukishikilia kanula kwa mkono wako ulio na glavu, ondoa plasta au chochote kinachoshikilia kanula kwa kutumia mkono huo mwingine. Ukitumia pamba safi isiyo na unyevunyevu kushikilia juu ya sehemu iliyodungwa, toa kanula kisha ufinye kwa vidole vyako kwenye sehemu hiyo kwa dakika moja au mbili. Pangusa sehemu hiyo kwa antiseptiki au alkoholi ili kuondoa viini vyovyote vinavyoweza kuwa vimekaribia shimo lilodungwa. Ngozi ikikauka, funika sehemu hiyo kwa plasta iwapo unayo.

Kila wakati, hakikisha kuwa kanula imetoka yote kisha uitupe salama kwenye chombo kisichoweza kutobolewa kwa urahisi.

22.3.1 Kuanzisha utaratibu wa ufuatilizi

22.4  Kuingiza katheta ndani ya kibofu