22.4.2 Hatua katika utaratibu wa kuingiza katheta

  • Je, ni jambo gani la kwanza unafaa kufanya kabla ya kufungua kifurushi chochote safi?

  • Kwa takriban sekunde 15, osha mikono yako kabisa kwa sabuni na maji.

    Mwisho wa jibu

Baada ya mgonjwa wako kuwa tayari na kufahamu matukio yatakayofuata, na vifaa vyako vimetayarishwa, vaa glavu safi kisha upanguze karibu na vulva na eneo la nje ya vulva ukitumia mchanganyiko wa antiseptiki au alkoholi, ukianzia kwenye uwazi wa urethra ukielekea upande (Mchoro 22.8a). Ikiwa hauna mchanganyiko wa antiseptiki, safisha eneo hili kikamilifu ukitumia sabuni na maji.

Mchoro 22.8 (a) Panguza sehemu ya karibu na vulva na periniamu kwa pamba iliyotumbukizwa ndani ya alkoholi. (b) Kwa upole, vuta labia kubwa ili kuona uwazi wa urethra kisha uingize katheta.
  • Unafikiri ni kwa nini ni muhimu kupanguza eneo hili ukianzia uwazi wa urethra kisha kuelekea upande wa nje?

  • Hatua hii huzuia kupanguza viini vya maradhi kutoka sehemu za periniamu kuelekea kwenye uwazi wa urethra. Ukipanguza kuelekea urethra, viini hivi vinaweza kubebwa hadi ndani ya mwili wakati katheta inapoingizwa.

    Mwisho ya jibu

Tumia mkono wako usio na nguvu nyingi kuvuta labia kubwa nyuma ili uwazi wa urethra uonekane. (Unaweza kurejelea mchoro wa kina kuhusu sehemu ya nje ya uke katika Mchoro wa 3.2 katika Kipindi cha 3. Lainisha katheta ya FK16 ikiwa una mafuta yanayofaa (usitumie kitu kingine) kisha uiingize polepole kwenye uwazi wa urethra (Mchoro 22.8b).

Punde tu baada ya katheta kuingia vizuri kwenye kibofu utaona mkojo ukitiririka kwenye katheta. Tumia sirinji kuingiza milimita 5 ya maji safi kwenye mrija unaoelekea kwenye puto; jambo hili litafanya kifuko hiki “kifure” na kusababisha katheta kushikilia kwenye kibofu hivyo haiwezi kutoka wakati mgonjwa anatembea (tazama Mchoro 22.9). Vuta katheta kwa utaratibu ili kuhisi jinsi ilivojishikilia kwenye kibofu.

Mchoro 2.9 Sehemu nusu ya kaviti ya pelvisi ya mwanamke ikionyesha katheta ilivyojishikilia kwenye kibofu kufuatia kufurishwa kwa puto la katheta.

Unganisha katheta na neli safi ya kupitishia mkojo ili mkojo utiririke kwenye kifuko cha kukusanyia. Hakikisha kuwa kifuko hiki kimewekwa chini ya kibofu, la sivyo mkojo hautatiririkia ndani ya kifuko. Ikiwa hauna kifuko safi cha kukusanyia, basi acha mkojo utiririkie kwenye chombo safi. Mbinu hii huitwa mfumo 'wazi' na huwa na hatari ya maambukizi kupitia katika njia ya mkojo hadi katika kibofu. Kwa kawaida, njia ya mkojo inafaa kuwa ya mfumo 'uliofungwa' huku mkojo ukitiririka ndani ya kifuko safi.

Punde tu baada ya kukamilisha utaratibu huu, mpe mwanamke huyu rufaa hadi katika kituo cha afya cha kiwango cha juu. Ikiwezekana, andamana naye.

22.4.1 Vifaa vya kuingizia katheta ndani ya kibofu

22.4.2 Utunzaji wa ujumla wa mtu aliyeingizwa katheta