Muhtasari wa Kipindi cha 22

Katika kipindi cha 22 umejifunza kuwa:

  1. Matibabu ya kudunga viowevu mishipani huhitajika kwa mwanamke mjamzito ili kuchukua nafasi ya viowevu vinavyopotezwa kufuatia kuvuja damu nyingi.
  2. Matibabu ya kudungia viowevu mishipani huhusisha; kufahamu jinsi ya kukusanya vifaa muhimu, kutambua sehemu ya kudunga mshipa, kuingiza kanula mishipani na kuidhibiti na kudumisha kiwango cha kasi ya mtiririko wa viowevu katika mfumo wa damu ya mwanamke.
  3. Sababu za kusitisha matibabu ya kudungia viowevu mishipani ni pamoja na: shinikizo la damu na mpigo wa moyo kurejea hali ya kawaida, viowevu kuvujia ndani ya tishu na karibu na sehemu iliyodungwa badala ya kuenda mishipani, dalili za maambukizi karibu na sehemu iliyodungwa au mwanamke akipata viowevu vingi kupita kiasi na anaonyesha ishara ya kuwa moyo au mapafu yake yanaweza kuwa yameathirika.
  4. Kuingiza katheta ndani ya kibofu huhusisha kutia mpira safi au mrija wa plastiki ndani ya kibofu kupitia kwenye urethra ili kuondoa mkojo. Utaratibu huu ni muhimu kibofu kikifura kutokana na kizuizi kinachozuia mwanamke kukojoa kwa njia ya kawaida, kwa mfano, wakati wa leba iliyodumu kwa muda mrefu au iliyozuiliwa.
  5. Katheta hushikishwa kwenye kibofu kwa kudungia maji safi kwenye puto ya katheta ili kufurisha na kufanya ijishikishe ndani ya kibofu.
  6. Mfumo uliofungwa ni muhimu katika kukusanyia mkojo. Mfumo wazi unaweza kusababisha maambukizi kuingia ndani ya kibofu kupitia kwenye mrija.
  7. Utaratibu wa kudhibiti maambukizi unafaa kuzingatiwa kila wakati unapopeana matibabu ya kudungia viowevu mishipani au unapoingiza katheta ndani ya kibofu; Nawa mikono kabisa kabla na baada ya taratibu hizi, vaa glavu safi na upanguze sehemu ya ngozi inayokaribia eneo la kuingizia katheta au ya kudungia viowevu ukitumia mchanganyiko wa antiseptiki au alkoholi kabla ya kuingiza kanula au katheta ya mkojo.
  8. Hakikisha kuwa umemweleza mgonjwa yale unayotaka kufanya kabla ya kufanya taratibu hizi, na umweleze umuhimu wa kusaidiwa kwa njia hiyo.
  9. Punde tu baada ya kukamilisha matibabu haya, mpe mwanamke rufaa hadi katika kituo cha afya cha kiwango cha juu haraka iwezekanavyo. Ikiwezekana, andamana naye.

Maswali ya Kujitathmini ya Kipindi cha 22